Msemaji wa Ikulu ya Rais Manoah Esipisu amesema kuwa Rais Kenyatta atasafiri kwenda Addis Ababa nchini Ethiopia, kuhudhuria mkutano wa mwaka huu wa viongozi wa nchi na serikali wanachama wa muungano wa Afrika.
Rais anatarajiwa kufafanua vilivyo msimamo wa Kenya kuhusiana na masuala mengi ya bara hili.
Akizingumza na wanahabari baada ya mkutano wa viongozi wa serikali mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Esipisu alisema kuwa viongozi wa Afrika wanatarajiwa kujadili hali ilivyo nchini Burundi, Sudan Kusini na Somalia, huku akisema itakuwa bayana kuwa mpango wa kukadiria amani na usalama katika bara la Afrika unafaulu.
Ameongeza kuwa masuala mengine ambayo yatajadiliwa ni pamoja na uimarishaji wa ushikamano baina ya mataifa ya bara la Afrika na Kenya na jinsi Afrika inavyoweza kupata mabilioni ya dola yaliotengwa na jamii ya kimataifa kwa shughuli za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
“Rais anatarajiwa kujadili mengi kuhusu misimano ya Kenya katika kutafuta suluhu la kuweka amani nchini Burundi katika Kongamano hilo la mwaka kwani mataifa mengi yataunga pamoja kulishauri taifa la Burundi kusitisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwani mapigano hayo yamechangia mauaji na umwagikaji wa damu,” alieza Esipisu.
Kwenye mkutano huo Esipisu amehoji kuwa mwanzoni mwa mwezi Februari serikali inatarajiwa kumkaribisha Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri ambapo atakuwa anafanya ziara yake ya kwanza nchini ambapo viongozi wakuu wa serikali na Rais huyo wa Misri watajadili masuala muhimu ikiwepo kuimarisha na kupanua biashara.
Amesisitiza kuwa masuala ya usalama yatajadiliwa kwani Rais huyo ameahidi kusaidia Kenya kuimarisha usalama ili kuboresha biashara kwani taifa la Misri hutegemea sana majani chai kutoka humu nchini.