Share news tips with us here at Hivisasa

Rais Uhuru Kenyatta amehimizwa kuzingatia katiba pindi anapofanya maamuzi yoyote ya kiserikali au uteuzi wa nyadhfa mbalimbali za serikali.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Ijumaa, afisa wa maswala ya dharura katika shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini MUHURI Fahad Changi, alisema kwamba watetezi hao hawapingi juhudi za rais za kuimarisha utendakazi wa serikali, ila lazima azingatie katiba.

Kulingana na Changi, Rais Uhuru hapaswi kuwatenga wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi nchini kwa kuwa wana uwezo wa kulihudumia taifa hili sawia na viongozi wa wanaume.

Changi amesema kwamba wanawake wengi humu nchini wana uwezo wa kutekeleza majukumu yao barabara sawia na wanaume,  hivyo basi akamtaka rais kuliteua upya baraza hilo la mawaziri nchini ili kuangazia katiba jinsi inavyoangazia haki za wanawake katika uongozi nchini.

“Tunamtaka rais kuzingatia katiba ya nchi pindi anapofanya maamuzi ya kiserikali au kuteua viongozi mbalimbali serikali kwani kutokana na hilo basi atakuwa anampa nafasi ya uongozi mwanamke kwa asilimia kubwa badala ya kutuea wanawake kidogo kama alivyofanya katika uteuzi wake wa baraza la mawaziri,” alisema Changi.

Shinikizo hizo zinajiri huku bunge la kitaifa likijiandaa kuwapiga msasa mawaziri na makatibu katika wizara mbalimbali waliyoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kumiliki wizara mbalimbali serikalini.