Share news tips with us here at Hivisasa

Rais Uhuru Kenyatta ameondoa ada ya visa wanaotozwa watalii wakigeni wenye umri wa miaka chini ya 16 katika hatua inayolenga kuimarisha sekta ya utalii nchini.

Akizunguma mjini Mombasa siku ya Jumanne wakati wa uzinduzi wa kivutio cha English Point Marina, Kenyatta alisema hatua hiyo itawapunguzia gharama watalii wanaondamana na familia zao wanapozuru nchini.

Rais vilevile alielekeza kuwa ada ya kuegesha magari pia ipunguzwe kutoka shilingi 9,215 hadi shilingi 6,143, huku akimuagiza waziri wa uchukuzi kuanzisha mchakato wa kuifanyia mabadiliko sheria ya utozaji ushuru kabla ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Kenyatta aliongeza kuwa serikali inajituma kuhakikisha kuwa inaimarisha ukuaji wa sekta ya utalii kwa kuboresha miundo msingi, usalama na kufanya kazi kwa karibu na wadau wa sekta hiyo.

"Tutafanya kazi na sekta ya kibinafsi kufanikisha maendeleo kama haya ili kuuokoa uchumi wetu na kuboresha sekta ya utalii ambayo ilikuwa imeanza kuzama," alisema Rais.

Uhuru aidha alisema kuwa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Malindi na Jomo Kenyatta itarahisisha shughuli za uchukuzi na kuiwezesha serikali kuwahudumia wageni wengi.