Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumatatu alifanya ziara ya ghafla katika makao makuu ya shirika la feri nchini Likoni Kaunti ya Mombasa. 

Wakazi wa kaunti hii wamekuwa wakilalamikia huduma duni zinazotolewa na shirika hilo kila uchao, lakini inakadiriwa kuwa ujio wa rais huenda ukawa ndio mwanzo wa mwisho wa masahibu yao. 

Akiandamana na waziri wa utalii Najib Balala, pamoja na mbunge wa eneo bunge la Likoni Masoud Mwahima, Rais alikutana na wasimamizi wa shirika hilo akiwemo mkurugenzi mkuu Musa Hassan Musa. 

Akiongea na wanahabari baada ya mkutano huo, Mwahima alidokeza kuwa mkurugenzi wa shirika hilo la feri alipitia wakati mgumu alipoulizwa sababu zinazochangia huduma duni katika kivukio hicho. 

Rais naye pia aliabiri feri na kuvuka kutoka kisiwa cha Mombasa hadi Likoni. 

Katika azma ya kuboresha huduma za kivuko hicho, serikali ina mipango ya kupunguza msongamano na kutafuta njia mbadala itakayotumiwa na wakaazi wa Mombasa, kwani inapendekeza ujenzi wa barabara ya kando eneo la Changamwe, ambayo itaunganisha Pwani kusini na magharibi pamoja na Pwani kazkazini. 

Kutokana na safari hiyo, haijabainika hatua atakayoichukua rais kukabiliana na changamoto za kivukio hicho cha Likoni feri.