Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kukutana na maafisa wakuu wa usalama jijini Nairobi siku ya Ijumaa ili kujadiliana jinsi watakavyokabiliana na ugaidi nchini.
Nia ya mkutano huo itakuwa kuimarisha usalama wa nchi pamoja na kutambua changamoto kuu katika idara hiyo.
Maafisa hao pia wanatarajiwa kueleza mikakati itakayowekwa kuhusiana na ongezeko la tishio la ugaidi, kwenye mkutano huo utakaofanyika katika chuo cha mafunzo cha maafisa wa upelelezi eneo la South C jijini Nairobi.
Rais anatarajiwa kuondoka mjini Mombasa kuhudhuria kikao hicho licha ya taarifa kutoka kwa Msemaji wa Ikulu Manoah Esipisu kuwa shughuli za rais katika eneo la Pwani bado hazikamilika.
“Rais Uhuru Kenyatta atahudhuria kikao cha usalama jijini Nairobi kujadili maswala muhimu ya kiusalama pamoja na viongozi wakuu katika idara ya usalama nchini. Wanatarajiwa kuunda mikakati ya kukabiliana na magaidi nchini,” alisema Esipisu katika mkutano na wanahabari katika ikulu ya Rais mjini Mombasa siku ya Alhamisi.
Hii ndio itakuwa mara ya pili kwa Rais Uhuru kukutana na viongozi wakuu wa usalama tangu kuchaguliwa kwake mwaka 2013.