Mbunge wa Rongai Raymond Kipruto Moi Ijumaa alikashifu shirika la Mzalendo Trust ambalo limemworodhesha kama mmoja wa wabunge wasiochangia miswada na mijadala bungeni, akisema kuwa ripoti hiyo ni ya uongo.
Mnamo Alhamisi Mzalendo Trust ilitoa orodha ya wabunge na maseneta wapatao 27 ambao wamesalia kimya bungeni 2015, Raymond akiwa mmoja wao.
Hata hivyo akizungumza na mwandishi huyu kwa njia ya simu akiwa kaunti ya TransNzoia Moi alisema kwamba, shirika hilo linanuia kumharibia jina yeye pamoja na wabunge wengine kwa kuwapotosha wananchi kabla ya uchaguzi 2017.
“Hili ni shirika ambalo ninaamini limelipwa na watu fulani kuharibia mimi na wabunge majina. Wakati tukifunga bunge mwaka jana kabla ya kurejelea Februari tisa mwaka huu, nilizungumza sana bungeni kuhusu maswala ya mashamba, je hata hiyo hawakupata?” Moi alisema.
Alisisitiza kwamba amekuwa akichangia kwenye miswada muhimu bungeni jambo ambalo shirika hilo lingegundua kama lingekagua rekodi na nakala za bunge.
“Ni lini shirika hilo lilikuja kunihoji jinsi nachangia mijadala katika bunge? Kama wanataka kupima utendakazi wangu, waende eneo bunge la Rongai wajionee maendeleo,” aliongeza.
Baada ya Mzalendo Trust kutoa ripoti hiyo Alhamisi Machi 10,2016, seneta wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko alikuwa wa kwanza kupinga habari hizo kwenye ukurasa wa Facebook.