Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Naibu wa Rais William Ruto sasa ameingilia kati sintofaamu zilizoko baina ya magavana na manaibu wao huku akiwashurutisha kufanya kazi pamoja, la sivyo hawatachaguliwa tena.

Huku akikiri kuwa sintofaamu hizo zimepelekea huduma kwa wakenya kufifia, Ruto amesema kuwa kulikuwa na njia za mbadala za kutatua maswala ibuka na wala si hadharani.

Akiwahutubia manaibu wa magavana wakati wa kongamano lao mjini Naivasha Alhamisi, naibu Rais alikiri kuwa katiba mpya haijafafanua vyema majukumu ya manaibu hao.

“Tunajua kuwa katiba haijafafanua kwa mapana majukumu yenu, lakini jambo halitatuliwi kwa malumbano. Ushirikiano na mazungumzo ndio huleta suluhisho la jambo lolote lile,” alisema Ruto.

Kutokana na hayo, Ruto ametoa changamoto kwa bunge la seneti kuharakisha kujadiliwa kwa miswada miwili itakayobaini majukumu yao kisheria.

Hata hivyo, kiongozi huyo amesema kuwa serikali ya kitaifa imejitolea kuhakikisha kuwa ugatuzi umetekelezwa, na kuongeza kuwa kufikia sasa takriban shilingi bilioni 693 zimetolewa kwa miradi ya maendeleo kwenye kaunti zote nchini.