Ukusanyaji wa ushuru katika kaunti ya Nakuru umeimarika mara dufu kutokana na utumizi wa teknolojia za kisasa.
Gavana wa kaunti hio Kinuthia Mbugua alisema kuwa serikali yake kwa sasa inakusanya shilingi bilioni 2.1 kila mwaka, kando na ilivyokuwa awali ambapo shilingi bilioni 1.2 ndizo zilikuwa zikikusanywa.
Mbugua alisema kuwa wanabiashara wengi katika kaunti hiyo wanalipa kodi kutumia huduma tofauti za kisasa kama Mpesa na kupitia benki, na hivyo kupunguza foleni kubwa kwenye afisi za kaunti hiyo.
Hata hivyo Mbugua alikiri kuwa serikali yake ina uwezo wa kukusanya shilingi bilioni sita kila mwaka, ikizingatiwa wametambua maeneo ambayo hayajakuwa yakitozwa ushuru.
”Hapa Naivasha kuna biashara nyingi kama hoteli, matatu, ukulima, kati ya zingine. Ushuru wote wa manispaa za miji yote wakati tulianza ugatuzi Nakuru, ilikuwa 1.2B, lakini ikaenda chini hata zaidi. Hapo tuliona tuanze huduma za kisasa za kukusanya pesa, na sasa tumefikisha bilioni 2.2, na pengine ni Nairobi tu ambayo iko mbele yetu kuokota ushuru,” Mbugua alisema.
Afisa msimamizi wa mauzo kutoka kwa Safaricom Rita Okuthe, alisema kuwa wataangalia jinsi ya kurekebisha, kuinua na kudumisha hadhi ya viwanja vitatu vya michezo katika kaunti ya Nakuru, ikiwemo Afraha Stadium na vingine viwili katika miji ya Kuresoi na Naivasha.
“Tumekubaliana kuweka mkataba wa kuanzisha mbinu za kushirikiana kuokota ushuru, lakini pia jinsi ya kuimarisha viwanja vitatu vya michezo, kimoja hapa Naivasha, Nakuru, na uwanja ambao unanuiwa kujengwa upya huko Kuresoi,” alisema.