Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Meli ya Ms Insignia iliyo na zaidi ya watalii elfu moja imetia nanga katika Bandari ya Mombasa kutoka mataifa mbali mbali ulimwengini baada ya mataifa ya magharibi kuondoa marufuku ya raia wao kutozuru humu nchini na husanan eneo la pwani.

Hii ni baada ya Meli Mv Nauticia iliyokuwa na zaidi ya watalii elfu moja vile vile kutia nanga katika bandari ya Mombasa wiki iliyopita.

Haya yanajiri baada ya serikali kupitia idara ya usalama na wizara ya utalii nchini kuimarisha usalama wa taifa hili na kuwavutia watalii zaidi kuzuru humu nchini.

Akiongea na wanahabari katika Bandari ya Mombasa siku ya Jumanne baada ya kupokea watalii hao, Mkurungenzi mkuu wa Bodi ya Utalii nchini Muriithi Ndegwa alisema kwamba hatua hiyo imejiri baada ya sekta ya utalii kwa ushirikiano na KPA, Serikali ya kaunti ya Mombasa na seriklai kuu kujizatiti kuimarisha sekta hiyo iliyokumbwa na changamoto.

Kulingana na Ndegwa, kuwasili kwa watalii hao humu kutainua kwa kiwango kikubwa sekta ya utalii sawia na kubuni ajiri kwa vijana.

Alisema kwamba watalii hao watazuru mbuga za wanyapori mbalimbali na vituo vya kutalii mjini Mombasa.

“Tunameona tukipokea watalii kwa mara ya pili sasa baada ya kuwasili kwa meli ya Mv Nauticia wiki iliyopita. Tuna matumaini kuwa sekta ya utalii itaimarika kwa asilimia kubwa na kufungua ajira kwa vijana baada ya kukumbwa na changamoto,” alisema Ndegwa.

Kwa upande wake Afisa mkuu wa mawasiliano katika Halmashauri ya Bandari ya Mombasa Haji Maseno alisema kwamba Halmashuri ya Bandari KPA imetenga kima cha shilingi milioni 100 za kukaribati eneo la kupumzika kwa watalii wanazuru katika bandari hiyo.

Watalii hao kutoka mataifa ya Ushelisheli, Uingereza, Marekani, ubelgiji na baadhi ya mataifa mengine ulimwenguni wataelekea kisiwani Zanzibar nchini Tanzania baada ya ziara yao humu nchini.