Sekta ya Utalii inatarajiwa kuimarika zaidi msimu huu wa likizo kufuatia ongezeko la watalii wanaozuru Ukanda wa Pwani.
Kulingana na Afisa Mkuu wa Chama cha Wamiliki na Wahudumu wa mahoteli katika ukanda wa Pwani Sam Ikwaye, wadau hao wanatarajia kati ya asilimia 80 hadi 90 ya wageni kutoka nje ya nchi na wa humu nchini, ambao watazuru ukanda huo ili kujivinjari.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Ikwaye alisema kwamba mikakati mwafaka imeandaliwa kuona kwamba sekta hiyo ya utalii inarejea hali yake ya hapo awali kufuatia kukumbwa na changamoto.
Akisema kwamba kuwasili kwa meli mbili za Watali za ‘MS- Nautica’ na ‘MV-Isgnia’ katika bandari ya Mombasa hivi majuzi ilikuwa ishara kamili ya kuimarika kwa sekta ya utalii.
“Tunatarajia kupata wageni kujivinjari eneo hili la Pwani ama asilimia zaidi ya 80 kwani utalii kwa sasa umeanza kuimarika na matumaini yetu ni kuwa kutafaidika zaidi,” alisema Ikwaye.
Afisa huyo alihimiza maafisa wa polisi kuzidisha oparesheni za kiusalama kote Pwani ili kuhakikisha kwamba eneo hilo lina mazingira bora na tulivu zaidi kwa watalii na wenyeji kujivinjari.
“Tunawahimiza maafisa wa usalama kuzidi juhudi zao za kuimarisha usalama ili kuona kwamba wageni wanaozuru eneo la Pwani wako salama,” aliongeza Ikwaye.