Seneta wa Nakuru James Mungai Kiarie amedai kuwa kuna baadhi ya viongozi wa serikali ya kaunti hiyo ambao huenda wana akunti za benki katika mataifa ya ugeni.
Akizungumza na mwandishi huyu mjini Nakuru siku ya jumatatu, Seneta Jemo kama anavyofahamika, alidai kwamba wakuu hao wa kaunti wameficha pesa za umma katika mataifa ya ulaya.
Ijapokuwa hakutaja kiwango hicho anachodai kimefichwa ulaya, alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kwamba wananchi wanaendelea kuathirika katika maeneo ya mashinani kwa kukosa huduma za kimsingi, huku viongozi wengine wakiendelea kujitakia makuu na kunufaika kutokana na pesa za mwananchi.
Kama mojawapo ya wajibu wake wa kufanya uangalizi wa kaunti ya Nakuru.
Amesema atayaandikia mataifa hayo ya kigeni barua ili pesa hizo alizodai zimefichwa katika mataifa hayo ya ulaya, zizuiliwe na wenye kuficha pesa hizo wakamatwe na wafunguliwe mashtaka.
Lakini naibu gavana Joseph Ruto imeyakanusha madai hayo na kumtaka Seneta huyo atoe ushahidi alio nao.
Aidha bwana Ruto alisema kuwa matamshi ya seneta huyo yananuia kuwapotosha wananchi.