Share news tips with us here at Hivisasa

Kufuatia tetesi kuibuka kuwa baadhi ya mawakala wananua watu kutoka eneo la Bonyunyu na Charachani katika kaunti ya Nyamira ili kuwasajili kama wapiga kura katika kaunti ya Kisii, Seneta wa kaunti ya Nyamira Okong'o Mong'are amejitokeza kushtumu vikali hali hiyo.

Akihutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumapili, Mong'are alisema kuwa hatua za baadhi ya viongozi wa kisiasa kuwarai wapiga kura kutoka katika kaunti zao kujisajili katika kaunti zingine ni uoga wa wanasiasa wanaohofia kushindwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.

"Haya maneno ya baadhi ya wanasiasa kujitokeza kununua watu ili kuhakikisha kuwa wametoka katika kaunti hii na kujisajili kama wapiga kura kule Kisii ni hujuma kwetu," alisema Mong'are.

"Na pia naona kama wanaofanya hayo ni wale wanaohofia kushindwa kwenye uchaguzi mkuu ujao,” aliongeza Mong'are.

Mong'are aidha aliwarai wakazi wa kaunti ya Nyamira kutokubali kununuliwa ili kujisajili katika kaunti zingine kwa kuwa hali hiyo itawanyima haki ya kuchagua viongozi wanaowataka.

"Ni ombi langu kwenu kutokubali kununuliwa ili kujisajili katika kaunti zingine kama wapiga kura kwa maana hali hiyo itawanyima nafasi ya nyinyi kuwachagua viongozi mnaowataka,” aliongezea Mong'are.