Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar amejitokeza na kueleza sababu kuu za kukosa kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa kitaifa wa 'Mwangaza Mitaani' uliozinduliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta siku ya Ijumaa katika uwanja wa Makadara, Kaunti ya Mombasa.
Omar alieleza kuwa kama mwanaharakati wa haki za binadamu, hajaona sababu za kuhudhuria uzinduzi huo ilihali hakuna uhakika wa usalama kwa wananchi licha ya kuwepo kwa taa hizo za kuweka mwangaza.
Akizungumza siku ya Jumamosi katika hafla ya kusheherekea maisha ya Sheikh Munir Mazrui kama mtetezi mkongwe wa haki za binadamu nchini, iliyoandaliwa na shirika la Haki Afrika katika makavazi ya Fort Jesus, Omar alitaka wakaazi kuimarishiwa usalama.
Aidha, aliongeza kuwa wananchi wameshindwa kutembea nyakati za usiku kwa hofu ya ukosefu wa usalama ama kuhangaishwa na maafisa wa polisi katika oparesheni zao.
Sherehe hiyo ilihudhuriwa na wanaharakati mbalimbali wa utetezi wa haki za binadamu nchini ikiwemo Jaji Mkuu Dkt Willy Mutunga, Gavana wa Makueni Prof Kivutha Kibwana miongoni mwa wengine.