Share news tips with us here at Hivisasa

Seneta wa Kaunti ya Tana River Ali Bule amepigwa marufuku kuzuru eneo la Kanagoni, Kaunti ya Kilifi, ambako jamii ya Wagiriama inaishi, hadi pale kesi ya uchochezi inayomkabili itakapotamatika.

Mahakama ilielezwa kuwa mnamo Julai 15, 2015 katika Ukumbi wa Hurura, kaunti dogo la Garsen, Bule anadaiwa kutamka maneno yanayodaiwa kutenganisha jamii kwa misingi ya ukabila.

Akitoa uamuzi huo siku ya Jumatatu, Hakimu Mkuu Diana Mochache alimtaka seneta huyo kutozungumzia kuhusu kesi hiyo kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, hadi uamuzi wa kesi hiyo utakapotolewa.

Uamuzi huo unajiri baada ya naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa, Alexendra Muteti, kuiomba mahakama kumzuia Bule kuzuru eneo hilo kwa kuhofia usalama wa wakazi wa eneo hilo.

Aidha, Hakimu Mochache alimtoza Bule dhamana ya shilingi milioni moja ama Sh500,000 pesa taslimu.

Bule alikanusha mashtaka hayo na kesi yake itasikilizwa Disemba 9, 10 na 11,2015 ambapo mashahidi 18 wanatarajiwa kutoa ushahidi wao.