Seneta wa Kaunti ya Uasin Gishu Isaac Melly alifika mbele ya mahakama ya Nakuru siku ya Alhamisi kujibu shtaka la kuzua vurugu katika Chuo Kikuu cha Eldoret.
Haya yanajiri baada yake kukosa kufika mbele ya mahakama mnamo Octoba 22, 2015 alipotakiwa kujibu shtaka hilo ambapo mahakama ilielezwa kwamba seneta huyo alikuwa nje ya nchi.
Kesi hiyo iliahirishwa wakati huo baada ya wakili wake kutoa ombi hilo huku akitaka kesi hiyo isikizwe mteja wake atakaporejea nchini.
Upande wa mashtaka unadai kuwa Seneta Isaac Melly, pamoja na wengine ambao hawakuwa mbele ya mahakama, walizua vurugu na kusababisha uharibifu wa mali ya Chuo Kikuu cha Eldoret, mnamo Februari 12, 2015.
Seneta Melly alikana shtaka hilo huku wakili wake Christopher Mitei akiomba mahakama imwachilie mteja wake kwa bondi.
Hakimu mkuu Doreen Mulekyo alikubali ombi hilo na kumwachilia kwa bondi ya Sh100,000 na mthamnini wa kiasi sawia.
Kesi hiyo itaskizwa Januari 25 na 26, 2016.