Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali kupitia Wizara ya Elimu itasambaza maji safi katika shule zote za umma nchini katika siku za hivi karibuni, hatua inayolenga kuimarisha mazingira ya masomo kwa wanafunzi.

Akizungumza katika hafla ya kufuzu kwa mahafali wa Chuo cha kutoa mafunzo ya elimu cha Kamwenja huko Nyeri siku ya Ijumaa, Waziri wa Elimu, Fred Matiang'i, alisema kuwa ni jambo linalokera kuwaona wanafunzi wakitembea umbali wa kilomita kadhaa wakitafuta maji safi, muda ambao wangetumia darasani.

Aidha, waziri huyo alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuzuia maambukizi ya magonjwa ya kipindupindu pamoja na homa ya matumbo yanayosababishwa na kunywa maji machafu.

Hii itakuwa afueni kwa shule nyingi nchini hususan katika ukanda wa Pwani ambapo mapema mwaka huu, shule nyingi zilipitia changamoto ya ukosefu wa maji baada ya bodi ya maji katika eneo la Pwani kusitisha huduma zake kwa madai ya malimbikizi ya madeni.

Aidha, waziri Matiang’i alisema kuwa serikali ina mpango wa kuwaajiri walimu 5,000 katika kipindi cha mwaka wa fedha ujao ili kuukabili uhaba wa walimu nchini.