Serikali ya Kaunti ya Mombasa imeanzisha harakati za kuzoa taka katika mitaa ya kaunti wakati wa jioni, kama njia moja ya kuweka mazingira bora.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hatua hiyo pia ni moja ya mikakati na utaratibu wa Kaunti ya Mombasa kuhakikisha kuwa hakuna usumbufu nyakati za kutekeleza shughuli hiyo ya uzoaji taka, na usafishaji wa jiji kwa jumla.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, mkuu wa idara ya mazingira katika Kaunti ya Mombasa Tendai Lewa, alisema kuwa huwa vigumu kwa wahudumu kutekeleza kazi za usafi wakati wa mchana, kwa kuwepo kwa shughuli nyingi.

Alisema kuwa hatua hiyo imechukuliwa mahusus kuleta utaratibu na kuwarahisishia kazi wahudumu waliotwika jukumu la kusafisha jiji.

Lewa alisema kuwa nyakati za jioni huwa rahisi wafanyakazi hao kuondoa uchafu mtaani, ikizingatiwa kuwa wafanyibiashara wengi huwa tayari wameenda majumbani mwao.

“Sharti wakaazi pamoja na wafanyibiashara kufanikisha shughuli hiyo na kuepuka kutupa taka ovyo kanda kando mwa barabara, ili kuwapa wahudumu hao kazi rahisi wanapotekeleza shughuli yao ya kusafisha mitaa,” alisema Lewa.

Aidha, alionya kuwa yeyote ambaye anajihusisha na utupaji taka kiholela ataandamwa na sheria.

Alisisitiza kuwa bado sheria ambayo iliundwa na serikali ya kaunti dhidi ya watupaji taka ipo na itaendelea kuwatafuta wavunja sheria.

Wakaazi wa mitaa ya kaunti hiyo ambao waliongea na mwandishi huyu, walipongeza hatua hiyo na kusema italainisha shughuli ya biashara.

Wakaazi hao walisema kuwa itakuwa rahisi kuondoa taka kwa sababu hamna watu wengi mitaani nyakati za usiku.