Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakulima kutoka kaunti ya Nyamira wana sababu ya kutabasamu baada ya taifa la Czech Republic kufanya kikao cha pamoja ili kuimarisha soko la zao la chai kwenye mataifa ya kigeni.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Gavana John Nyagarama alishukuru taifa hilo kwa ushirikiano wa karibu na taifa la Kenya, huku akiongeza kusema ana hakika kuwa taifa hilo litanunua zao la chai kutoka Nyamira ili kuimarisha mapato ya wenyeji.

“Taifa la Czech lina uhusiano mzuri na taifa la Kenya, na nina hakika kuwa kupitia mazungumzo haya tutaweza kuliuzia taifa la Czech chai yetu, na kwa sababu ya kuwa na washirika dhabiti kutoka maitaifa ya uropa, nina hakika kuwa tutawasaidia wakulima kujistawisha,” alisema Nyagarama.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Czech Republic Yogan Zukov alisema kuwa serikali yake imejitolea kufanya biashara na serikali ya kitaifa na zile za kaunti kama njia mojawapo ya kuafikia sheria zilizowekwa na taifa hilo kwa mataifa ya kigeni, na ili kupata mazao bora yanayohitajika na taifa la Czech.

“Nina furaha hii leo kwamba baada ya mazungumzo haya, wananchi wa taifa langu watapata nafasi ya kuyanunua mazao kama chai bila yakupitia njia za madalali na tunatarajia kufanya kazi kwa pamoja na kaunti zote nchini,” alisema Zukov.

Gavana Nyagarama aidha aliongeza kuwa serikali yake itafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kwamba inawatafutia wakulima wanaokuza zao la chai.

“Serikali yangu itafanya juhudi bidii kuhakikisha kwamba inawatafutia wakulima wa chai soko bora kuuza mazao yao ili kuhakikisha kuwa madalali wanaonunua chai kutoka kwa wakulima kwa bei ya chini wamezuiliwa kuendesha biashara zao,” aliongezea Nyagarama.