Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi wa eneo la Bamburi katika eneo bunge la Kisauni mjini Mombasa wanalalamikia hali duni ya miundo msingi na wameitaka hali hiyo itatuliwe kwa haraka.

Wakazi hao wakiongozwa na wanaharakati wa vijana eneo hilo Salim Mayumbe walisema kwamba hali duni ya barabara imedumu kwa miaka mingi mno bila ya viongozi husika kuchukua hatua zozote mwafaka za kukabiliana na  hali hiyo na wakasisitiza hali hiyo kurekebishwa.

Akizungumza katika eneo hilo la Bamburi siku ya Jumanne, Mayumbe alihoji kwamba ni aibu kwa wakazi wa eneo hilo kukabiliwa na hali duni ya miundo msingi, ilhali maeneo mengine ya kaunti ya Mombasa yameboreshwa kimiundo msingi.

Mayumbe aliitaja hali hiyo duni ya miundo msingi kama iliyohitilafiana pakubwa na shughuli za uchukuzi, kibiashara na za kiuchumi kwa jumla, huku wakitoa wito kwa uongozi wa kaunti ya Mombasa kuliangazia zaidi eneo hilo katika hali ya miundo msingi.

"Tunaiambia serikali ya kaunti ya Mombasa kurekebisha barabara za eneo la Bamburi ili kuboresha shughuli za kibiashara katika eneo hilo sambamba kuinua uchumi wa Mombasa," alisema Mayumbe.

Picha: Shughuli ya uboresheji wa barabara katika kaunti ya Mombasa ikiendelea. Viongozi wa kaunti wamekosolewa kwa kulitenga eneo la Bamburi. /Businessdaily.