Serikali ya Kaunti ya Kisii imeombwa kujenga chuo cha anuwai katika eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini ili kuinua viwango vya elimu katika eneo hilo.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Marani, Josephat Osoro, aliyeongea kwa niaba ya wakazi wa eneo bunge hilo alisema wamekuwa wakikosa chuo hicho cha anuwai, na kuwalazimu kutafuta mafunzo katika eneo bunge zingine badala ya kuwa na chuo chao.
Kulingana nao, idadi kubwa ya wanao humalizia masomo katika darasa la nane na wengine katika kidato cha nne na kushindwa pa kujiunga ili kujiendeleza kwa mafunzo ya kiufundi wakati wanahitaji mafunzo hayo, ambayo yameonekana ya kulipa katika siku za hivi maajuzi.
“Tunaomba serikali ya Kaunti ya Kisii, kupitia gavana wetu James Ongwae kuinua viwango vya elimu katika eneo bunge hili la Kitutu Chache kwa kutufungulia taasisi hapa ili watoto wetu wapate mafunzo ya kiufundi,” alisema Osoro.
“Elimu ya vyuo vya anuwai iliweza kuwasilishwa kuwa chini ya uongozi wa serikali za kaunti, na kuna haja ya serikali kutekeleza majukumu yake kuhakikisha elimu hiyo imeboreshwa kikamilifu,” aliongeza Osoro.
Serikali ya kaunti hiyo ndio ina jukumu la kuitikia wito wa wakazi wa eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini na kuwajengea chuo hicho cha anuwai ili kuinua viwango vya elimu hasa katika sekta ya kiufundi.