Serikali ya Kaunti ya Kisii imeombwa kuleta maendeleo kwa manufaa ya wakazi.
Mbunge wa Bobasi alisema kuwa kuna baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo bado haijashugulikiwa kikamilifu katika baadhi ya sehemu za kaunti hiyo ya Kisii tangu serikali za ugatuzi zianzishwe nchini.
Akizungumza siku ya Jumapili katika kanisa la Nyamagwa, Steve Manoti aliomba serikali ya kaunti kufanya maendeleo na kutimiza ahadi ilizotoa hapo awali ili kunufaisha wakazi wa kaunti hiyo.
“Naomba serikali ya kaunti yetu ifanye maendeleo kwa kukarabati barabara zile ziko chini ya serkali ya kaunti, kuweka maji katika wadi zote, kushughulikia sekta ya afya na maendeleo mengine husika,” alisema Manoti.
Wakati huo huo, Manoti aliomba serikali hiyo kufungua zahanati nane zilizojengwa katika eneo bunge la Bobasi, kupitia pesa za ustawi wa maeneo bunge (CDF) zilizokamilika kujengwa mwaka wa 2013.
Manoti alisema ni jambo la kushangaza zahanati zinapojengwa na kumalizika kwa zaidi ya miaka miwili na kutofunguliwa ilihali wananchi wanahitaji huduma za matibabu.
“Naomba gavana wetu James Ongwae kufungua zahanati hizo nane zilizoko katika eneo bunge la Bobasi, ili wakazi waweze kupokea huduma za kimatibabu,” alisema Manoti.