Serikali ya kaunti ya Kisii imepongezwa kwa kupunguza ada ya waendeshaji bodaboda.
Waendeshaji bodaboda katika Kaunti ya Kisii walistahili kulipa Sh300 kila mwezi lakini walisusia kulipa ada hiyo kwa muda mrefu, na kulazimisha serikali ya kaunti kupunguza ada hiyo hadi Sh200 kila mwezi.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne mjini Kisii, wahudumu hao, wakiongozwa na mwenyekiti wa waendeshaji bodaboda katika kituo cha Uchumi, James Nkoge, walipongeza serikali kwa kuitikia wito na malalamishi yao na kupunguza ada hiyo.
“Sisi waendeshaji bodaboda tuliagizwa kulipia kibandiko cha pikipiki Sh300 kila mwezi lakini bei hiyo ilikuwa ya juu sana. Tumefurahishwa na hatua ya serikali ya kaunti kupunguza ada hiyo mpaka Sh200,” alisema Nkoge.
Wakati huo huo, waendeshaji bodaboda hao waliomba serikali ya kaunti hiyo kuwakarabatia barabara zile ambazo hazipitiki ili kuimarisha sekta ya uchukuzi.
“Kile tunahitaji sasa ni kukarabatiwa barabara zile ziko chini ya uongozi wa Kaunti ya Kisii ili sekta yetu ya uchukuzi imarike kwani huwa vigumu kuendelea na biashara yetu kunaponyesha,” alisema Jairus Nyakoe, mhudumu wa bodaboda.