Share news tips with us here at Hivisasa

Kama njia moja ya kuzuia mkurupuko wa ugonjwa wa miguu na midomo kwa mifugo wakati huu wa msimu wa mvua, idara ya kilimo katika kaunti ya Nakuru itazindua shuguli ya kutoa chanjo ya bure kwa mifugo wote wakiwemo punda.

Afisa wa mifugo katika kaunti ndogo ya Naivasha, Enos Amuyunzu amesema kuwa wanapania kuwachanja mifugo wote ili kuwakinga dhidi ya maradhi yanayoweza kuenea haraka wakati wa mvua nyingi.

Akiongea Alhamisi afisini mwake mjini Naivasha, Amuyunzu alisema kuwa chanjo hiyo itakayotolewa bure pia itajumuisha punda.

Aliwataka wafugaji wote kuhakikisha mifugo wao wamepokea chanjo hiyo .

“Wakati wa mvua huwa kuna hatari kubwa ya kutokea maradhi ya mifugo na hii inatubidi kuwakinga mifugo wetu kwa kuwachanja,” alisema.

“ Tutazindua shuguli ya chanjo katika maeneo ya wafugaji katika kaunti ndogo zote za Nakuru tukianza na Naivasha na itakuwa bure kwa hivyo kila mfugaji anaombwa kuhakikisha kuwa mifugo wake wamepokea chanjo hiyo,” aliongeza.

Amuyunzu alisema kuwa chanjo hiyo itasaidia kukabiliana na magonjwa ya kuambikizana katika mifugo haswa katika maeneo yaliyo na hatari ya kukabiliwa na magonjwa hayo ya mifugo.