Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Haki Afrika limedizi kuishinikiza serikali kushikilia msimamo wake wa kutowaondoa wanajeshi wa KDF nchini Somalia, ili kuimarisha zaidi usalama wa taifa.

Afisa mratibu wa mipango katika shirika hilo Francis Auma, amesema kuwa iwapo serikali itazingatia pendekezo hilo na kupuzilia mbali kauli ya baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaopendekeza kuondolewa kwa wanajeshi hao, basi taifa hili litaimarika kiusalama.

Auma alisema kwamba Rais Uhuru Kenyatta anafaa kutolegeza kamba katika kujitolea kupiga vita ugaidi, kwani hiyo ndio changamoto kubwa la usalama wa taifa hili.

Akiongea katika kongamano la vijana mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Auma alisema kwamba shirika hilo litaendelea kuishinikiza serikali kuongeza wanajeshi zaidi wa KDF nchini Somalia, kuhakikisha kuwa usalama umeimarishwa zaidi nchini humo na katika mipaka ya Kenya na mataifa jirani.

“Tunaiomba serikali kutolegeza msimamo wake wa kukabiliana na magaidi hasuasan Kundi la al-Shabaab na kuliagamiza kabisa kundi hilo kwani limekuwa tishio la usalama kwa taifa hili. Tunawaomba Wakenya kuunga mkono juhudi za serikali kuimarisha usalama,” alisema Auma.

Pendekezo la mwanaharakati huyo limejiri huku Rais Kenyatta akiahidi kushirikana na serikali ya Nigeria katika kukabiliana na makundi ya kigaidi na kulinda usalama wa wananchi.