Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Serikali kuu na ile ya Kaunti ya Mombasa zimehimizwa kuangazia vyema haki za watoto ili kumlinda dhidi ya dhulma za kijinsia.

Mwenyeti wa kamati ya bunge kuhusu Vijana, Jinsia na Michezo katika kaunti ya Mombasa Serah Nyamvullah amesema kuwa iwapo swala hilo halitapewa uzito, basi mtoto katika jamii atazidi kuhangaika.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Nyamvullah alisema kuwa vipengele vya katiba vimeangazia vyema kuhusu haki za watoto, na iwapo sheria hiyo itatekelezwa, jamii itafaulu katika kumtekelezea mtoto mahitaji yake.

"Tunaitaka serikali kuzingatia vile vipengele mhimu katika katiba vinavyomjali mtoto na kumlinda dhidi ya dhulma ili kumwezesha kupata msingi bora wa kiafya, kielimu na hata mavazi," alisema Nyamvullah.

Nyamvullah, ambaye pia ni mwakilishi maalum wa bunge hilo, aliongeza kuwa kushuhudiwa kwa visa vingi vya dhulma za kijinsia ikiwemo ubakaji na kuangamizwa kwa watoto kumetokana na jamii kukosa kufahamu haki za watoto wao.

Kiongozi huyo ameahidi kuzuru mashinani na kuielimisha jamii kuhusu haki za mtoto sambamba na kuielewa kuhusu katiba jinsi inavyomuangazia mtoto kisheria.