Share news tips with us here at Hivisasa

Maafisa wa idara ya elimu katika kaunti za Pwani pamoja na serikali kuu wameombwa kuanzisha uchunguzi wa kina katika shule za msingi na Upili kutokana na kukithiri kwa visa vya mimba za mapema.

Akiongea na mwanahabari wetu siku ya Jumatano katika mkutano wa elimu mjini Mombasa, mkaazi wa Mwaluphamba kaunti ya Kwale Salim Kapombe amesema kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wa kike wanaopachikwa mimba imechangiwa na umaskini na kamwe hakuna hatua zozote za kisheria zinachukuliwa.

Kapombe amependekeza hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika sambamba na wataalum ya kiafya kuzitembea shule hizo na kuwapima wanafunzi ili kufahamu matatizo yanayochangia na kuwasaidia wasichana hao kufanikisha masomo yao.

"Tunaiomba serikali kuhakikisha kuwa inawachukulia hatua kali za kisheria wahusika ili kupunguza kukithiri kwa visa kama hivi kwani imevunja ndoto za watoto wa kike kutimiza masomo yao," alisema Kapombe.

Kapombe ameongezea kuwa umaskini ndio chanzo kikubwa kwa wanafunzi wa kike kupachikwa mimba kwani hatua hiyo imedhihirisha wazi wazazi hushindwa kuwatimiza mahitaji muhimu ya watoto wao wa kike.

"Chanzo kikubwa kwa mambo haya ni umaskini ambao wazazi wenyewe ndio wamechangia kutokana na kutotimiza mahitaji muhimu ya watoto wao wa kike ili kuwazuia kujihusisha na masuala kama haya," alieleza Kapombe. 

Kaunti ya Kwale, Mombasa na Kilifi zinaongozwa kwa visa vya mimba za mapema kwa watoto wadogo wa shule hali ambayo imechangia pakubwa watoto hao kutofanikisha masomo yao na kuzorotesha viwango vya elimu.