Waziri wa Utalii kaunti ya Kwale Adam Sheikh ameitaka serikali kuu kutafuta suluhu la kudumu katika kivuko cha feri cha Likoni ili kuzuia msongamano.
Akiongea na wanahabari baada ya kukutana na wadau wa sekta ya utalii mjini Mombasa siku ya Ijumma, Adan alisema kuwa iwapo serikali itajitolea kikamilifu kukabiliana na changamoto zinazokikumba kivuko hicho basi kwa kiwango kikibwa sekta ya utalii itaimarika.
Ameilaumu Serikali kuu kwa kukosa kuangazia changamoto zinazoshuhudiwa katika kivuko hicho, akisema kuwa kuzembea kwa baadhi ya viongozi kumechangia huduma duni.
Alieleza kudidimia kwa sekta ya utalii eneo la kusini mwa Pwani kutokana na kushuhudiwa kwa huduma duni katika kivuko hicho licha ya kuwa kiunganishi cha biashara baina ya nchi jirani ya Tanzania na Kenya.
“Serikali kwa kiwango kikubwa imechangia kudidimia kwa sekta ya utalii pamoja na viongozi wakuu katika shirika la huduma za feri nchini kutokana na kuzembea kuwajibikia mjukumu yao," alisema Adan.
Shinikizo zake zinajiri siku tatu tu baada ya kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Huduma za Feri nchini Musa Hassan Musa, pamoja na maafisa wengine wakuu wawili.