Serikali imelaumiwa kwa kushindwa kukabiliana na visa vya udanganyifu wa mitihani ya kitaifa, hali iliyotajwa kuchangia kwa wanafunzi kukosa matokeo yao ya mitihani ya KCSE ya mwaka uliopita.
Akizungumza siku ya Jumapili katika mkutano wa wadau wa sekta ya elimu mjini Mombasa, Katibu wa Chama cha Kuppet katika Kaunti ya Kwale, Makenzi Tuki, alisema kuwa serikali kuu ndio iliyochangia pakubwa kwa wanafunzi wa kidato cha nne kuhusika katika udanganyifu wa mitihani ya KCSE.
Makenzi alisema kuwa iwapo serikali inataka kusitisha visa vya udanganyifu wa mitihani ya kitaifa, basi lazima waanze kukabiliana na maafisa wa sekta ya elimu wanaohusika moja kwa moja na wizi wa mitihani, kwani wanafunzi hupata makaratasi hayo kutoka kwa maafisa hao.
“Serikali ndiyo ilichangia kukithiri kwa visa vya udanganyifu wa mitihani ya KCSE mwaka jana. Ni lazima kwa serikali kuanza kukabiliana na maafisa wahusika kutoka kwa baraza la mitihani ndio tuweze kuzuia wizi wa mitihani,” alisema Makenzi.
Wakati huo huo, aliwataka wadau wa sekta ya elimu nchini na katika ukanda wa Pwani kuhakikisha kuwa wanaimarisha viwango vya elimu kwa kuwawekea wanafunzi mazingira bora ya elimu, pamoja na vifaa vya masomo vya kisasa.
Kaunti ya Isiolo pekee ndio ilikosa kuorodheshwa katika orodha ya kaunti zilizohusika katika udanganyifu, huku wanafunzi 5,101 kukosa matokeo yao ya kitaifa ya KCSE.