Jamii ya Maasai wameilaumu serikali kuu kwa kuwanyang’anya ardhi yao ambayo imemilikiwa na mababu zao tangu jadi, huku wakiitaja kitendo hicho kama dhuluma na ubaguzi.
Jamii hiyo pia imeelezea kusikitishwa kwao na waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaiseri ambaye wanasema hajawatetea vilivyo huku wakiendelea kudhulumiwa haki yao ya umiliki wa shamba.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa chama cha ODM tawi la Nakuru Peter Ole Osono, jamii hiyo pia imedokeza kuwa baadhi ya wanyakuzi wa ardhi yao hutoka kaunti za kericho na Bomet, huku usalama wao pia ukihatarishwa.
"Ni jambo la kuhuzunisha kuona serikali imetutenga sisi jamii ya Maasai kwa kukosa kutulinda kutoka kwa wanyakuzi wa ardhi zetu. Kwa miaka mingi sasa jamii hii imeishi kwa hofu ya kushambuliwa na jamii nyinginezo. Ndiyo maana tunaiomba serikali kuchunguza jambo hili na kuwachukulia hatua wale ambao wanachochea vita hivi," Ole Osono alielezea.
Viongozi hao walikuwa wakizungumza na wanahabari siku ya Jumamosi jijini Naivasha baada ya hafla ya mazishi ya mmoja wao kusitishwa kufuatia kesi iliyowaslishwa kortini na kampuni ya ADC Farm ya kusitisha shughuli hiyo kufuatia mzozo wa shamba alikokuwa azikwe marehemu.
Mwaniaji wa kiti cha mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Narok Lydia Ntimama kwa upande wake amedhibitisha kuwa jamii hiyo itasimama kidete ili kupinga mipango yoyote ya kuwahamisha kutoka mashamba yao kama inavyodaiwa.
"Sisi kama jamii ya Maasai hatutatishika na vitisho vya kututoa kwenye mashamba yetu ya Ndabibi ambayo imemilikiwa na wazee wetu wa kale. Hatutakubali mtu yeyote kutoka nje ya jamii hii atapewa ardhi yetu," Ntimama alielezea.