Walimu wakuu katika kaunti ya Nyamira wamejitokeza kuitaka serikali ya kaunti kwa ushirikiano na ile ya kitaifa kuezeka vifaa vya kuthibiti radi kwenye paa za shule.
Hii ni kufuatia visa vya radi kuripotiwa kuwasababishia majeraha na hata pia maafa watu hasa wanafunzi wanapokuwa shuleni.
Akihutubu kwenye shule yakitaifa ya wasichana kule Sironga siku ya Jumapili wakati wa hafla ya mkutano wa walimu wakuu kujadili jinsi yakuthibiti majanga shuleni mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Ramba Patrick Onyambu ni kuwa kuna visa vya maafa ya wanafunzi na hata walimu ambavyo vimekuwa vikisababishwa na radi hali aliyosema inaweka maisha ya wanafunzi kwenye hatari.
"Jamii ya Abagusii ni jamii mojawapo inayoishi kwenye nyanda za juu za ardhi hali inayotuweka kwenye hatari yakuathirika kutokana na madhara yeyote yanayo sababishwa na radi na inastahili serikali ya kaunti na ile ya kitaifa zishirikiane kuhakikisha hali hiyo inathibitiwa ili kuokoa maisha ya wengi," alisema Onyambu.
Onyambu aidha alisema wanafunzi wanastahili kuwa watulivu hasa wakati mvua ya ngurumo za radi inaponyesha hali aliyosema itasaidia kuthibiti visa vya wanafunzi kupigwa na radi.
"Ni himizo langu kwa wanafunzi kuwa watulivu hasa wakati mvua inaponyesha kwa kuwa ripoti zimekuwa zikionyesha kuwa hali ya wanafunzi kucheza cheza nje wakati mvua inaponyesha ndio chanzo cha radi kuwapiga wanafunzi," alihimiza Onyambu.
Haya yanajiri baada ya mkulima mmoja huko Ramba kuwapoteza ng'ombe wake pale ambapo radi ilipoangamiza mifugo hao wenye kima cha shillingi elfu 200,000 siku chache zilizopita.