Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa bodi ya Elimu katika kaunti ya Kisii Henry Onderi ameomba serikali ya kitaifa kutuma pesa zinazofadhili elimu ya bure kwa wakati unaofaa ili kuendeleza masomo jinsi inavyostahili na majukumu mengine ya kielimu.

Wito huo umetolewa baada ya serikali mara nyingi kuchelewa kutuma pesa hizo kwa shule jambo ambao hupelekea masuala fulani ya kielimu kutoafikiwa kwa wakati unaofaa.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Kisii Onderi aliomba serikali kutuma pesa hizo mapema kwa shule ili kufadhili elimu ya bure.

Kulingana na mwenyekiti huyo shule nyingi zimekuwa zikishuhudia kuchelewa kwa pesa kutoka serikali ya kitaifa jambo ambalo halipendezi na hata kurudisha masuala ya kielimu nyuma kwa kutoafikiwa kwa muda ule unaotakikana.

“Naomba serikali ya kitaifa kutorudia makosa yale ya kuchelewesha kutuma pesa za kufadhili elimu ya bure kwa shule za humu nchini. Naomba watume mapema ili kuendeleza elimu na majukumu mengine ya serikali,” alisema Onderi.

Hata hivyo Onderi aliomba walimu wakuu wa shule zote katika kaunti ya Kisii kuonyesha haki kwa wazazi na kwa wanafunzi kwa kutoongeza karo ya shule kiholela kwani wanawaumiza wanafunzi na wazazi.

“Mwalimu mkuu wa shule hastahili kuamka asubuhi na kufikiria kiwango cha karo mwanafunzi anastahili kulipishwa kwa shule, hiyo ni kunyima mwanafunzi haki ya masomo,” aliongeza Onderi.

“Naomba kila mwalimu mkuu wa shule kutoongeza karo kwani itakuwa gharama kubwa kwa wazazi,” alisisistiza Onderi.