Mashirika mbalimbali ya kijamii yamejitokeza kupongeza uamuzi wa mahakama wa kufungua akaunti za benki za mashirika ya utetezi wa haki za kibinadamu Muhuri na Haki Afrika.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Ijumaa, afisa wa nyanjani wa shirika la kijamii la Kenya community support centre Mwalimu Rama, alisema kwamba uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo siku ya Alhamisi umedhihirisha kuwa mahakama inawajali wananchi.
Rama alisema kwamba serikali inafaa kuchunguza kwa kina utendakazi wa mashirika yao kabla ya kuyahusisha na maswala ya kufadhili makundi ya kigaidi kutokana na fedha wanazopata kutoka kwa wafadhili, kwani hatua hiyo inazidi kuyakandamiza mashirika yao.
Afisa huyo wa nyanjani aliwashtumu maafisa wa upelelezi kwa kuyahusisha mashirika yao na ugaidi na kufungwa kwa akaunti zao akisema kwamba taifa hili ni huru na katiba inamuangazia vyema mwananchi ya jinsi mashirika ya kijamii yanavyofaa kufanya kazi.
"Tunapongeza hatua ya mahakama jinsi ilivyotoa uamuzi wake bila ya kuegemea upande wowote, na kuagiza kufunguliwa kwa akaunti za mashiriki hayo,” alisema Rama.
Hatua ya afisa huyo imejiri baada ya mahakama kuu mjini Mombasa kuagiza kufungwa kwa kesi ya kuzuiliwa kwa akaunti za mashirika ya Muhuri na Haki Afrika kutokana na kuhusishwa na tuhuma za kuwafadhili vijana kujiunga na makundi ya kigaidi.