Serikali na idara ya mahakama zimepongezwa kwa kushughulikia kesi zinazowahusu watoto kwa wakati ufaao.
Michael Sasi kutoka shirika la 'Mission in Action', ambalo hushughulikia maswala ya watoto anasema kuwa mrundiko wa kesi za watoto umepungua katika mahakama.
Katika mahojiano ya kipekee mjini Nakuru, Sasi alisema kuwa ni hatua mwafaka katika kuhakikisha haki kwa watoto.
Aliongeza kuwa mahakama maalum za kushughulikia kesi za watoto zimebuniwa Nakuru, na ni jambo la kutia moyo sana.
"Ni jambo la busara kwani sasa kuna mahakama ya kesi za watoto, na pia katika idara ya polisi kuna kitengo maalumu kwa ajili ya kesi za watoto," alisema Sasi.
Wakati huo huo, ametoa wito kwa kila mmoja katika jamii kuheshimu haki za watoto, huku akisisitiza kuwa ni hatia kwa mtoto yeyote yule kudhulumiwa.