Share news tips with us here at Hivisasa

Baada ya msongamano wa magari ya uchukuzi na yale ya umma katika eneo la Taru kufikia zaidi ya kilo mita 60, Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Ali Joho ameitaka serikali kuingilia kati na kutatua tatizo hilo.

Akizungumza na wanahabari katika eneo la msongamano huo, Joho alisema kwamba msongamano huo mkubwa umeathiri shughuli za kiuchumi katika Kaunti ya Mombasa, na msongamano wa makasha katika bandari ya Mombasa ukizidi kulemaza shughuli za bandari hiyo.

Joho alisema kwamba ni vigumu kwa shughuli za kibiashara kunawiri katika kaunti hiyo, huku wizara ya uchukuzi na maafisa wa trafiki wakikosa kuchukua hatua za kuudhibiti msongamano huo.

Gavana aliitaka serikali, kupitia wizara ya uchukuzi na miundo msingi pamoja na halmashuri ya barabara nchini kuibuka na mbinu mwafaka za kukarabati barabara hiyo ili kuona kwamba swala hilo linasuluhishwa.

“Tunaitaka serikali kuu, kupitia wizara ya uchukuzi na miundo msingi kuingilia kati swala hili na kuibuka na suluhu la kudumu, na kama ni upanuzi wa barabara hatua za dhurura zichukuliwe na kupunguza changamoto hizi,” alisema Joho.

Joho aidha amedhihirisha hofu kwamba huenda hali hiyo ya msongamno wa magari katika barabara hiyo kuu inayotokana na kuwepo kwa mbovu ya barabara na uzembe wa Mwanakandarasi katika eneo hilo la Taru ukaathiri pakubwa sekta ya utalii nchni.

“Sisi tunasema kwamba tunahofia sekta ya utalii itakumbwa na changamoto kubwa sana iwapo tatizo hili halitasuluhishwa kwa dharura kwa sababu msimu huu wa likizo ya Desemba ndio unapokea watalii wengi Mombasa,” aliongeza Joho.

Hapo jana, abiria wengi waliokuwa wameabiri mabasi na wale madereva wa masafa marefu walilazimika kulala na kusalia katika eneo hilo la Taru kwa siku mbili kutokana na msongamno huo mkubwa uliyosababisha na kuharibika kwa barabara.