Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwenyekiti wa muungano wa Wanawake wa Kiislam nchini 'Kenya Muslim Women Alliance', Farida Rashid, amesema kuwa serikali inastahili kuvunjilia mbali baadhi ya vitengo vya uongozi nchini ili kugharamikia miradi muhimu ya kimaendeleo.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano katika mkutano wa wanawake, Rashid alisema kuwa iwapo serikali inahitaji kusonga mbele kimaendeleo, basi lazima baadhi ya viongozi wanaoshikilia nyadhifa mbalimbali zisizokuwa na umuhimu wowote kwa wananchi kuvunjiliwa mbali ili kumfaidi mwananchi.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa baadhi ya nyadhifa za serikali kuu za kaunti zinashikiliwa na zaidi ya afisa mmoja ilhali kuna masuala muhimu kama ujenzi wa barabara, hospitali, uimarishaji wa sekta ya utalii na kazi kwa vijana yamesaulika kutokana na kupanda kwa gaharama ya maisha.

"Tunaiomba serikali pamoja na zile za kaunti kuhakikisha kuwa inapunguza makujumu yake ya kusimamia baadhi ya idara na vitengo vya uongozi, ili kuwasaidia Wakenya katika kugharamia masuala muhimu mashinani,” alisema Farida.

Mwanaharakati huyo amependekeza serikali kuliangazia suala hilo na kuwafaidi zaidi Wakenya mashinani katika masuala muhimu ya kimaendeleo ili taifa hili kusonga mbele kiuchumi.