Waendeshaji malori wanaosafirisha mizigo hadi katika nchi jirani kupitia barabara inayofungua eneo la Afrika Mashariki na kati wamehimiza serikali kujenga eneo la kuegeza magari katika kituo cha kibiashara cha Salgaa ili kupunguza ajali katika eneo hilo.
Kwenye taarifa kwa wanahabari hapo jana Jumatatu, madereva wa malori hayo wamedai ajali nyingi zinazotokea katika barabara ya Kibunja-Salgaa zinaweza zikazuiwa iwapo kuna eneo la kuegesha magari katika eneo hilo la Salgaa.
Wameongea kwamba katika matukio mengi, magari yanayotoka Eldoret hugonga magari ambayo yameegeshwa kandokando ya barabara kuu katika kituo cha kibiashara cha Salgaa, haswaa wakati breki zao zinapopata matatizo au wakati ambapo madereva wanakosa udhibiti wa magari yao.
Madereva hao sasa wameonyesha kusikitishwa kwao na siasa ambazo zimeonekana kushamiri katika eno hilo, kiasi kwamba Benki ya Dunia iliondoa mpango wake wa hapo awali wa kugharamia ujenzi wa eneo la kuegesha magari kama ilivyoahidiwa kwenye serikali ya Narc.
Huku akionya kuwa wafanyibiashara katika kituo hicho pia wako katika hali ya hatari, madereva hao sasa wameshauri serikali kujadiliana na wakazi wa eneo hilo ili kuafikiana kuhusiana na mpango wa kufidiwa ili kuzuia kuibuka kwa mzozo punde tu ujenzi huo utakapokamilika.
Kwa sasa, zaidi ya malori mia tano husimama katika kituo cha kibiashara cha Salgaa kwa usiku mmoja.