Serikali imeshinikizwa kuingilia kati swala la mizozo ya ardhi katika eneo la Pwani na kutafuta suluhu la kudumu ili kusitisha kuenea kwa maswala ya dhuluma za kihistoria.
Kiongozi wa vijana wa Kimijikenda katika eneo la Pwani Nguma Charo amesema kwamba viongozi wa kisiasa lazima washirikiane na tume ya kitaifa ya ardhi inayoongozwa na Muhamed Swazuri, na kulitatua swala hilo ili kumwezesha mpwani aishi kwa amani.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Nguma alisema kwamba iwapo viongozi hao wataimarisha ushirikiano na tume hiyo inayotambua vyema swala la dhuluma za kihistoria eneo la pwani, basi mizozo mingi ya ardhi itasitishwa.
Amemtaka Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kulichukulia swala hilo kwa uzito na kutafuta suluhu kabla ya migogoro ya ardhi katika ukanda huo kuzua mgawanyiko baina ya wananchi.
"Tunawaomba viongozi wetu tuliyowachangua kushirikiana vyema na tume ya kitaifa ya ardhi na kutafuta suluhu la kudumu kuhusiana na dhuluma za kihistoria ili maswala ya mizozo ya ardhi iweze kusitisha katika eneo hili la pwani," alisema Nguma.
Kauli ya kiongozi huyo wa vijana imejiri siku chache tu baada ya waziri wa ardhi nchini Profesa Jacob Kaimenyi kuwatembelea wakazi katika Shamba la Waitiki huko Likoni, mjini Mombasa.