Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwenyekiti wa kiwanda cha majani chai cha Kebirigo ameziomba serikali za kaunti kushirikiana na halmashauri ya KTDA ili kuimarisha kilimo cha majani chai.

Mwenyekiti huyo alisema mara nyingi halmashauri ya KTDA hujitegemea kwa shughuli nyingi jambo ambalo limepelekea wakulima wa majani chai kutofaidika kutoka zao lao kufuatia ukosefu wa ushirikiano na serikali.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano mjini Nyamira, David Kireri aliomba serikali za kaunti kushirikana na halmashauri hiyo ya KTDA ili wakulima kufurahia matunda ya zao lao.

Kireri aliomba serikali ya kitaifa kujaribu kila iwezalo kutafuta soko la majani chai katika nchi za ng’ambo ili kuwafaa wakulima.

“Tunaomba serikali itutafutie soko katika nchi za ng’ambo ili zao letu liwe likiuzwa kwa pesa ya juu na sisi wakulima tuweze kufaidika,” alisema Kireri.

Aliongeza, “Mara nyingi halmashauri ya KTDA hujitegemea katika shughuli nyingi na tunaomba serikali za kaunti ziweze kushirikina pamoja ili mkulima aweze kufaidika maana sekta ya kilimo iko chini ya uongozi wa kaunti.”

Aidha, Kireri aliowaomba wakulima wa majani chai kutouza zao lao kwingine na kulipeleka katika vituo vya ununuzi na kupima majani chai ili kupata pesa baada ya kila mwezi badala ya kukabidhiwa pesa za kila siku.

“Mkulima anapouza majani chai yake bila kupeleka mazao hayo katika vituo vyetu vya ununuzi, yeye hupata hasara kubwa maana hatapata mbolea, mshahara wa kila mwezi na hata pesa za ziada ambazo hutolewa kila mwaka,” alisema Kireri.