Share news tips with us here at Hivisasa

Zaidi ya shilingi milioni sita kutoka hazina ya CDF katika eneo bunge la Jomvu zimetengwa kuboresha huduma za kiafya.

Kulingana na Mbunge wa eneo hilo Badi Twalib, kati ya fedha hizo, shilingi milioni 1.5 zimetengwa kujenga ua katika Hospitali ya Kuu ya Jomvu ili kuzuia wanyakuzi wa ardhi kunyakua kipande cha ardhi ya hospitali hiyo.

Akizungumza katika eneo bunge la Jomvu mjini Mombasa siku ya Jumapili, Badi alisema kwamba fedha zingine ikiwemo shilingi milioni 4.5 kutoka hazina hiyo ya CDF zitatumika katika ujenzi wa makazi ya wauguzi na wahudumu wa afya kwa lengo la kuwasaidia wakazi kupata huduma bora.

Aidha, aliwashinikiza wakazi kuzidi kueleza changamoto wanazozipitia ili kuiwezesha kamati ya hazina ya CDF katika eneo bunge hilo kutenga fedha zaidi za kuboresha shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Hazina ya CDF katika eneo bunge langu la Jomvu imetumia fedha zake vizuri kwa sababu tumeanza kuboresha hospitali zetu ili kuhakikisha kwamba wakazi wetu wanapata huduma bora za afya. Ningependa kuwahimiza wakazi wa eneo bunge la Jomvu tushirikiane tufanye maendeleo,” alisema Badi.

Wakati uo huo, aliwatahadharisha wakazi dhidi ya kushiriki siasa za uchochezi akisema kwamba hatua hiyo huenda ikawagawanya wakazi kwa misingi ya kisiasa, na kuvuru mpango ya maendeleo katika eneo bunge hilo.

Mbunge huyo wa Jomvu aliahidi kushirikiana kwa karibu mno na wakazi wa eneo bunge lake ili kuona kwamba malengo ya demokrasia, uchumi na maendeleo yanafanikishwa.