Wafungwa kwenye magereza kote nchini watakuwa na nafasi ya kupiga kura ikiwa mapendekezo ya kamati moja ya bunge yatatekelezwa.
Kamati hiyo ya usalama wa kitaifa inataka wafungwa hao kupewa haki hiyo kama jinsi ilivyo kwa wakenya wengine.
Wanakamati wa kamati hiyo ambao walizuru gereza kuu la Naivasha Jumapili aidha walisema kuwa kulifaa kubadilishwa kwa sheria kadhaa ili kuwapa wafungwa hao haki hizo.
Kaimu mwenyekiti Grace Kiptum alisema kuwa watafanya marekebisho kwenye sheria ya magereza ili kuhakikisha kuwa wakenya wote wana haki hata kama wamo gerezani.
“Tutahakikisha kuwa sheria inabuniwa itakayowaruhusu wafungwa wote kupata haki hiyo ya kimsingi,” alisema Kiptum.
Naye mwenzake David Gikaria, ambaye pia ni mbunge alisema kuwa watahakikisha kuwa wafungwa hao wamepiga kura kama jinsi walivyofanya wakati wa kura ya maoni ya katiba mpya.
“Wakati wa kuchagua katiba mpya kila mwananchi wakiwemo wafungwa waliweza kupiga kura na tutahakikisha pia mwaka ujao pia hayo yanaafikiwa,” alisema Gikaria.
Kwa upande wake mbunge wa Wajir Magharibi Ahmed Abdikadir amesema kuwa watahakikisha kuwa wafungwa waliotiwa mbaroni kwa makosa ya ugaidi wametenganishwa na wenzao.
“Tunaendelea na mikakati ya kuhakikisha wafungwa waliofungwa kwa mashtaka ya ugaidi wanatenganishwa na wale wa mashtaka tofauti,” alisema Abdikadir.