Tangu bunge lipendekeze sheria ya bunge kuhusu mashirika ya kijamii udhamini kwa mashirika hayo kutoka katika mataifa ya kigeni umerudi chini.
Udhamini huo umerudi chini kwa kiwango kikubwa, ambapo baadhi ya mashirika hayo yanatishiwa kusambaratika.
Hayo ni kwa mujibu wa balozi Steven Tarus.
Tarus alisema kuna haja ya maoni ya wadau kuhusishwa katika marekebisho na kubuniwa kwa sheria husika ili kulinda mashirika ya kijamii ambayo huchangia katika maongozi mema na maendeleo ya kitaifa nchini.
Hata hivyo Tarus, ambaye ni mbunge wa awali wa Emgwen, alitaka mashirika ya kijamii kuajibikia fedha za udhamini kutoka katika mataifa ya kigeni na wadhamini wa humu nchini. Wakati huo huo mashirika yasiyokuwa ya kiserikali Uasin Gishu yanasisitiza kuwa yataendelea kuikosoa serikali kuhusiana na maswala yanayowahusu wakenya.
Mwenyekiti wa muungano wa mashirika hayo tawi la Uasin Gishu Joel Sawe alisisitiza kuwa hawatakubali kusalia kimya huku serikali ikienda kinyume na matarajio ya umma.
Akizungumza mjini Eldoret Alhamisi hii, Sawe alihoji kuwa licha ya serikali kuonekana kushtumu namna Mashirika ya kijamii yanavyoendesha shughuli zao, hilo halitaathiri utekelezaji wa majukumu yao.
"Iwapo serikali haitakuwa ikiendeshwa kwa njia inayomfaidi mkenya, sisi kamwe hatutabaki kimya ila tutatoa sauti na kushinikiza mambo kuendeshwa kwa njia inayofaa," alisema Sawe.
Afisa huyo hata hivyo alisisitiza kuwa wataendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali ili kufanikisha maendeleo kwa taifa la Kenya.
"Lengo letu ni kuona taifa linapiga hatua mbele na iwapo serikali imeanzisha miradi ya kumnufaisha mwananchi tutaunga mkono," alisema Sawe.
Kwenye hatua inayoonekana kulenga Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, serikali imekua ikiendesha harakati za kubuni sheria za kudhibiti shughuli na ufadhili wa Mashirika hayo.
Jaribio la kwanza halikufua dafu mwishoni mwa mwaka jana baada ya Bunge la kitaifa kupiga kura ya kupinga mswada ambao ulilenga kupunguza ufadhili wa Mashirika ya kijamii nchini kutoka mataifa ya kigeni hadi asilimia 15.