Kampeni rasmi imeanzishwa ya kuhakikisha kuwa vijana wanapata ushauri wa jinsi ya kujiepusha na itikadi kali, ugaidi pamoja na uhalifu na kukaa na amani miongoni mwa jamii.
Kwenye mahojiano na mwandishi habari huyu kwenye mkahawa wa kitalii wa Sarova Whitesands Resort siku ya Jumapili, Sheikh Ibrahim Lethome amesema kuwa tayari wameanzisha utaratibu huo wa kuwafikia vijana wote katika kaunti ya Mombasa na eneo la Pwani kwa jumla.
Naye Ramadhan Juma, ambaye ni mshirikishi wa shirika hilo la Brave amesema kuwa watafanya kila juhudi kwa kutumia mifumo mbali mbali kama makongamano pamoja na vyombo vya habari ili kuwafikia wahusika ambao ni vijana
“Tunajaribu kuwafikia vijana hawa kupitia kwenye makongamano ambayo tunafanya kote hata mashinani ili kuona kila mmoja anafikiwa, pia tunatumia vyombo vya habari ili kuwapata walengwa kwa ujumbe huo,” alisema afisa huyo.
Sheikh Abdullahi Waqo, ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa shirika hilo alisema kuwa tayari wamewahusisha vijana kutoka maeneo ya Pwani kaskazini mashariki na wanapania kutumia njia mbali mbali ili kuwafikia vijana wote nchini bila kubagua.
Shirika hilo litaendeleza kampeni hizo kwa siku 21 zijazo ili kusambaza ujumbe kwa vijana na vipi wanaweza kutumia nguvu zao kueneza amani na kujiepusha na masuala ya itikadi kali na kuacha kutumia dini vibaya.