Shirika lisilo la kiserikali la Crutches for Africa kutoka marekani limetoa zaidi ya viti vya magurudumu elfu mbili mia sita kwa walemavu katika kaunti ya Nakuru.
Shirika hilo, kupitia mkurugenzi wake, David Talbot, na mkewe Candice, limetoa shehena hiyo pamoja na vitu vingine vitakavyotolewa kwa walemavu bure.
Akiongea alipompokeza gavana Kinuthia Mbugua shehena hiyo, Talbot alisema kuwa shirika hilo linalenga kuhakikisha kuwa kila mlemavu katika kaunti ya Nakuru anapata vifaa vya kumwezesha kuendelea na shuguli zake za kila siku bila matatizo.
“Tunajua matatizo wanayopitia walemavu kwa kuwa hata mimi ni mmoja wao na ndiposa tumekuja hapa kuleta vifaa hivi kutoka kwa wahisani wa marekani,” alisema Talbot jumamosi.
“Mimi kama mlemavu ninayajua matatizo na ugumu tunayopitia na ndiposa mimi na mke wangu tutazidi kufanya kila tuwezalo kuwasaidia na mtuombee ili tupate shehena nyingine,” aliongeza mkurugenzi huyo.
Vifaa hivyo vitagawiwa walemavu katika kila kaunti ndogo kumi na moja za Nakuru.
Wengine waliohudhuria sherehe hiyo ni naibu gavana Joseph Rutto, mwakilishi wa walemavu katika bunge la kaunti Emma Mbugua na maafisa wakuu serikalini pamoja na wawakilishi wa walemavu.
Shirika la jitegemee linalosimamia walemavu katika kaunti ya Nakuru lilitakiwa kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vinagawanywa kwa njia ya wazi ili kuwafaidi walemavu wote.