Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Afisa wa elimu katika eneo la Gesima Robert Obiria amewataka wamiliki wa shule binafsi katika eneo hilo kusajili rasmi shule zao au shule hizo zifungwe mara moja.

Akihutubu wakati wa kukagua baadhi ya shule hizo siku ya Jumatano, afisa huyo alisema kuwa hatua hiyo itasaidia Wizara ya Elimu kuzitambua shule zinazo watapeli wazazi kwa kuwahaada kuwa wamewasajili wanao kwenye mitihani ya kitaifa.

"Tunataka kuona watoto wetu wakisajiliwa kujiunga na shule zinazo tambulika na serikali. Tunataka kuepukana na visa ambapo wanafunzi watahiniwa hugundua kuwa shule zao hazitambuliki pindi tu wanapo taka kujisajili kufanya mitihani ya kitaifa," alisema Obiria.

Afisa huyo aidha alizionya vikali shule zilizo na mazoea ya kuajiri walimu wasiohitimu kuwapa mafunzo wanafunzi, akihoji kuwa wamiliki wa shule husika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

"Sharti wasimamizi wa shule binafsi waajiri walimu waliohitimu na wala sio wanafunzi walio maliza masomo ya kidato cha nne kwa nia ya kutengeneza faida zaidi. Ni onyo langu kuwa watakao patikana na hatia watachukuliwa hatua kali za kisheria," alisema Obiria.