Vifijo, shangwe na nderemo vilishamiri kwenye shule ya upili ya wavulana ya Nyambaria baada ya shule hiyo kuibuka ya kwanza kwenye mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE katika eneo zima la Gusii kwa kupata alama ya wastani 10.18.
Akihutubia wanahabari ofisini mwake siku ya Alhamisi, mwalimu mkuu wa shule hiyo Gerald Orina alisema bidii ya wanafunzi na walimu darasani ndiyo iliyozalisha matokeo mazuri katika shule hiyo.
"Matokeo haya mazuri ambayo tumeyaandikisha leo hii hayajakuja kwa bahati tu ila kwa bidii na ushirikiano wa karibu kati ya walimu na wanafunzi na kwa hakika tunamshukru Mungu," alisema Orina.
Kwa upande wake mwanafunzi aliyeibuka bora katika shule hiyo Nelson Mandela, alisema kwamba angependa kujiunga na kikosi cha wanajeshi nchini huku akiwahimiza wanafunzi wenzake kutia bidii masomoni.
"Ni furaha kujua kwamba mimi ndio mwanafunzi wa kwanza kote katika kaunti ya Nyamira kwa kupata alama ya A yenye wastani wa maki 84, na ningependa kujiunga na kikosi cha wanajeshi ili nami nichangie katika kupambana na magaidi wa Alshabaab, ila ni himizo langu kwa wanafunzi wote kote nchini kutia bidii masomoni ili kufanikiwa maishani," aliongezea Mandela.