Share news tips with us here at Hivisasa

Mwakilishi wa wadi ya Bahati, kaunti ya Nakuru Peter Nderitu, amekemea siasa zinazochochewa na wachache wenye matakwa ya kibinafsi, katika miradi inayofadhiliwa na serikali ya kaunti.

Akizungumzia wananchi katika lokesheni ya Wanyororo B mnamo Ijumaa kitongoji cha Balaster, bw Nderitu alisema “siasa za wachache hazitazuia nifanye kazi ambayo inahitajika na imepitishwa na wananchi walio wengi.”

Alisema hayo baada ya akina mama watano na kijana mmoja kuzua kioja kwa kuzuia tinga la kaunti na lori la kusanya changarawe, kulainisha uwanja ambapo anatarajia kujenga shule ya chekechea, wakitaka changarawe hiyo imwagwe kwenye barabara za kijiji hicho, kinyume na makubaliano ya awali.

“Sisi tunataka umwage hiyo changarawe pale, afadhali hilo darasa likae lakini usibebe hii changarawe upeleke barabara zingine. Kwanza tengeneza barabara hizi ama ujenge darasa uwanja ukiwa hivyo,” alifoka mama mmoja.

Lakini Nderitu aliwataka kukumbuka kwamba mkutano wa umma ulifanyika mnamo Jumatatu, ambapo alieleza jinsi kazi hiyo itafanywa.

Tulikubaliana na wale ambao walikuwa kwenye mkutano kwamba huu uwanja unahitaji kuchimbwa ulainike, na barabara zitachimbwa. 

Kwa hizi barabara za kijiji hiki, hatumwagi changarawe nyingine kwa sababu tayari kuna milima ambayo itachimbwa ili barabara ilainike. Mchanga wa huu uwanja tutaupeleka wapi kama hamtaki ubebwe?” alihoji Nderitu.

Wazee wa kijiji hicho wakiongozwa na Daniel Karanja na chifu wa eneo hilo, waliwakemea akina mama hao kwa kusema wanazuilia maendeleo ambayo hawajapata tangu kupewa mashamba hayo, miaka 20 iliyopita.

“Kama hamtaki MCA afanye kazi yake kisheria, tutaandika pendekezo kwamba darasa hili lijengwe huko Wanyororo,” alisema chifu Macharia.