Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Polisi na maafisa kutoka kampuni ya kusambaza nguvu za umeme nchini, Kenya Power, mjini Naivasha wamewatia mbaroni washukiwa sita waliopatikana wakiiba katika mitambo miwili ya kusambaza umeme wa transfoma katika kijiji cha Mirera.

Inadaiwa washukiwa hao tayari walikuwa wameiba mitambo miwili ya transfoma na walikuwa katika harakati ya kufyonza mafuta kutoka kwa mitambo hiyo wakati wa kukamatwa kwao.

Afisa mmoja mwenye cheo cha juu kutoka kampuni hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina kwa misingi kuwa hakuwa na ruhusa ya kuzungumza na vyombo vya habari, alisema kuwa wanaendelea kupoteza mamilioni ya pesa kutokana na wizi wa mitambo hiyo muhimu katika usambazaji wa nguvu za umeme.

Alisema kuwa baadhi ya mashine ambayo imekuwa ikiharibiwa ni zile zenye volteji ya juu ambayo huwahudumia idadi kubwa ya wakaazi haswa wanaoishi mkabala na barabara ya Moi South Lake katika mji huo.

“Kupotea kwa nguvu za umeme ambayo tunashuhudia mara kwa mara hutokana na wizi wa mitambo ya transfoma na nawahimiza wakazi kuweza kuripoti watu wanaowashuku ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao,” alisema afisa huyo.