Spika wa Bunge la Kaunti ya Nakuru Susan Kihika amewashtumu wanasiasa kwa kile alichokitaja kama kuingilia maswala ya kibinafsi ya familia ya marehemu Kimani Kihika kuhusiana na urithi wa mali.
Haya yanajiri siku moja tu baada ya wajane saba wa marehemu Kihika kumshtumu Spika Kihika kwa madai kwamba anatumia umaarufu wake kurithi mali ya marehemu.
Katika kikao na wanahabari siku ya Ijumaa mjini Nakuru, Kihika akiwa ameandamana na nduguye Kungu Kihika na wanachama mbalimbali wa Bunge la Kaunti ya Nakuru, alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kwa maswala ya familia ya Kihika kuingiliwa na baadhi ya wanasiasa katika kaunti ya Nakuru.
Wakati huo huo, Kihika alisema kuwa familia ya marehemu Kihika haijawai kuwa na mzozo baina yao hadi pale baadhi ya wanasiasa kuingilia maswala ya urithi wa mali ya familia hiyo.
Matamshi hayo yaliungwa mkono na Kungu Kihika, ambaye ni nduguye Spika Kihika.
Wawili hao wameapa kushirikiana kutatua mzozo huo kinyumbani pasina kuingizwa siasa.
Katika kikao hicho, wanachama wanawake wa Bunge la Kaunti ya Nakuru akiwemo Emmah Mbugua anayewakilisha wanaoishi na ulemavu, wameapa kusimama kidete na Spika Kihika katika kutatua swala hilo.
Kwa mujibu wao, swala la kisiasa halifai kutumiwa kuwakandamiza wanawake walio katika uongozi.