Vijana kutoka kaunti ndogo ya Borabu walijitokeza kudhihirisha vipaji vyao kwenye uwanja wa Shule ya Upili ya Menyenya.
Akihutubia vijana hao siku ya Jumatatu, mbunge wa Borabu Ben Momanyi, aliyefadhili hafla hiyo, alisema kuwa hafla sawia na hiyo itakuwa ikifanywa kila mwaka na vijana watakaopatikana kuwa na vipaji mbalimbali watasaidiwa kukuza talanta hizo.
"Nina furaha kuona kwamba vijana wengi wana vipaji na talanta mbalimbali. Mimi kama mbunge nitahakikisha kuwa vijana watakaoibuka washindi kwenye tamasha hili wanafadhiliwa na uongozi wangu hadi waimarike kwenye taaluma zao,” alisema Momanyi.
Mbunge huyo aidha aliwaomba vijana kuimarisha vipaji vyao na kuwahimiza wazazi kuunga mkono taaluma zinazowafaa wanao badala yakuwalazimisha kufanya taaluma wanazozipendelea wazazi.
"Tunaishi kwa dunia huru na sharti watoto wapewe nafasi zakuchagua taaluma wanazozipenda badala yakulazimishwa na wazazi kufanya kazi wasizozipenda. Talanta kweli hulipa na mimi ni miongoni mwa watu ambao wamenufaika pakubwa kutokana na talanta zao,” alisema Momanyi.