Serikali ya kaunti ya Mombasa imezidi kusisitiza kuwa shughuli ya usafishaji mji katika nyakati za usiku utazidi kuendelea licha ya wafanyikazi wa kaunti hiyo kulalamikia usalama duni.
Kaimu waziri wa mazingira na raslimali za maji kaunti ya Mombasa Tendai Lewa Mtana, amesema kuwa mikakati ya kutekeleza shughuli hiyo ya ukusanyaji taka taka nyakati za usiku umekamilika.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Tendai amesema kuwa tayari shughuli hiyo imeanza maeneo ya Kongowea na Mkomani katika eneo bunge la Nyali huku akisema kuwa zoezi hilo litatekelezwa maeneo ya Likoni pia.
"Mikakati mwafaka imeidhinishwa na tayari maeneo ya Kaskazini mwa kaunti ya Mombasa tumeanza kusafisha taka usiku na tutaendelea mji hadi mji ili kuona kwamba kaunti yetu iko safi na iwavutie wageni wengi wanaolenga kuzuru Mombasa," alisema Tendai.
Wakati uo huo amewahakikishia usalama wakaazi pamoja na wafanyikazi wa kaunti hiyo wa kusafisha mji na kukusanya taka taka kwani maafisa wa polisi wameagizwa kushika doria kikamilifu.
"Tunajua kuwa wanyafikazi wetu wa kusafisha mji wako na hofu ya usalama wao, hilo tungependa kuwahakikishia kuwa usalama wao umezingatiwa na maafisa wa polisi watashika doria ili shughuli hiyo kufanyika bila wasiwasi wowote na tuokoe wakati," alieleza Tendai.